http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Saturday, May 11, 2013

MTABIRI: MABOMU MENGINE YAJA


MNAJIMU maarufu nchini, Maalim Hassan Yahya Hussein, amesema kuwa milipuko zaidi ya mabomu itatokea nchini mwaka huu.
Maalim Hassan ambaye ni mrithi wa kazi za aliyekuwa mnajimu maarufu Afrika, marehemu Sheikh Yahya Hussein, amefafanua kwamba milipuko mfano wa ule uliotokea Arusha wikiendi iliyopita, itaitikisa nchi mwaka huu.
Alisema, jambo hilo alilitabiri mapema na matokeo ndiyo yanaanza kuonekana, akaongeza kuwa milipuko ya mabomu inayokuja, italipua mpaka misikiti.
Maalim Hassan alisema, hali ya milipuko itaendana na majanga, siyo Tanzania tu bali duniani kote kwa sababu mwaka 2013, ulianza katika siku mbaya kinyota.
“Mwaka 2013 ulianza Jumanne. Kinyota, Jumanne ni siku ya mashaka, matatizo, vita, moto na malaika anayetawala siku hiyo ni Israeli mtoa roho. Isitoshe mwaka 2013 namba 1 ni nyota ya punda ambayo inawalenga viongozi, yaani watatofautiana sana.
“3 ni nyota ya mapacha ambayo inaashiria familia nyingi zitakuwa na matatizo, pia 1 ikijumlishwa na 3 inakuwa 4 ambayo ni nyota inayowalenga wazazi yaani vifo vya wajawazito vitakuwa vingi,” alisema Maalim Hassan na kuongeza:
“Yaani yanayotokea sasa ni sehemu ya utabiri nilioutoa lakini bado mengine yanaendelea, milipuko itaendelea kuwepo, watu kuuana kwa risasi kwa sababu Jumanne inatawaliwa na moto, hivyo watu wanatakiwa kumuomba Mungu sana kwani mwaka huu umeanza vibaya na siyo kwa Tanzania tu mambo haya yatatokea duniani kote.”
Kwa upande mwingine, Maalim Hassan aliwaasa viongozi hususan wale wa kidini, kuwa makini na kauli zao, vinginevyo zinaweza kuleta mifarakano ya kijamii kupitia imani zao.
“Kwa Waislamu na Wakristo, hekima na busara zitumike katika kuzungumzia mambo yanayoendelea, kwani kauli za vita zimekuwa zikitajwa sana na baadhi ya watu katika jamii tofauti na miaka iliyopita, hivyo umakini unatakiwa kuwa wa hali ya juu kwa viongozi ili kuepusha vita Tanzania,” alisema.
Kauli hiyo ya Maalim Hassan kuhusu marejeo ya utabiri wake alioutoa mapema mwaka huu, imekuja muda mfupi baada ya mlipuko wa bomu kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Arusha, lililoua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 70, pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali, Jumapili iliyopita.

No comments:

Post a Comment