TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: YA GODBLESS LEMA KUHUSIANA NA SUALA LA MGOMO WA WANAFUNZI ARUSHA
Jana majira ya saa nne asubuhi nilipokea taarifa kutoka Chuo cha
Uhasibu juu ya tukio la mauaji ya mwanafunzi yaliyotokea jana usiku kwa
kuchomwa kisu eneo karibu na chuo , nilipita Chuoni hapo baada ya
kusikia taarifa hiyo , nilikuta Wanafunzi wengi sana wakiwa
wamekusanyika pamoja wakiwa na jazba huku Kamanda wa Jeshi la Polisi
Wilaya akijaribu kuwasihi watulie wakati walipokuwa wanatafuta muafaka
wa kuzuia jazba ambayo ilikuwa ina lengo la kuandamana kwenda kwa Mkuu
wa Mkoa.
Nilipata faragha ya kuongea na Mwalimu aliyekuwa pale (
Dean of Student ) pamoja na OCD na wote walinieleza tatizo lilivyoanza
na kuomba nitumie busara kuzuia jazba na maandamano hayo yaliyokuwa
yamepangwa kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa niliongea na wanafunzi na
niliwasihi watulie na nilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Wilaya na
Mkuu wa Mkoa na kwa bahati nzuri nilimpata Mkuu wa Mkoa na kumweleza juu
ya kifo hicho na kile ambacho wanafunzi wanakusudia kufanya kuandamana
kwenda ofisini kwake. Nilimuomba afike ili aweze kutuliza hali hile na
pia atoe kauli juu ya tukio hilo baya la kuhuzunisha kwani ikizingatiwa
kuwa ni zaidi ya mara moja matendo kama haya yamekuwa yakitokea na
hakuna hatua zozote zimekuwa zikichukuliwa kuwahakikishia Wanafunzi
Usalama wao na mali zao.
Mkuu wa Mkoa pamoja na mimi kumpa
taarifa mapema aliahidi kufika mapema jambo ambalo halikufanyika na
wanafunzi walianza kuwa wakali na nilifanya jitihada na hekima za hali
ya juu kuvuta subira za wanafunzi hao ili Mkuu wa Mkoa afike . Baada ya
Mkuu wa Mkoa kufika Makamu wa Chuo aliniomba niwaandae wanafunzi
kumsikiliza Mkuu wa Mkoa na yeye alikwenda kumchukua Mkuu wa Mkoa na
kumpa mukutasari wa tukio zima na hali halisi ya kilichokuwa kinaendelea
na kimsingi Mkuu wa Mkoa alipofika Wanafunzi walitaka apande juu
kuongea mahali ambako tulitumia kama jukwaa kwa maongezi wakati wote
lakini badala yake mambo yafuatayo yalianza kutokea
1) Mkuu wa
Mkoa alikataa na kunitaka nishuke chini mahali alipokuwa yeye na timu
yake ya ulinzi na usalama Mkoa kwa kweli nilitii na nilipotaka kuongea
nae alinidharau na kuniambia hawezi kuongea na wanafunzi wahuni
wasiokuwa na nidhamu maneno ambayo yaliwatia wanafunzi hasira zaidi na
nilimsihi na kumuomba Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa (RSO) kumshawishi
Mkuu wa Mkoa kukubali kuongea nao kwani hali ilivyokuwa ni dhahiri
kwamba wanafunzi wale walikuwa na jazba ya hali ya juu na hivyo hekima
na unyenyekevu ndio ilikuwa njia pekee ya kutuliza hali hile.
2) Mkuu wa Mkoa alitoa masharti kwamba asingeweza kuongea nao bila
kipaza sauti na wanafunzi wote waende jengo lililokuwa karibu na Utawala
na wakisha kaa atakuja kuongea nao jambo ambalo wanafunzi waligoma kwa
imani kwamba jengo hilo lisengeweza kuchukua wanafunzi wengi na mimi
niliaga naondoka kwenda msibani na wanafunzi waligoma nisiondoke mpaka
watakapo sikilizwa na kwa kweli nilitii maombi baada ya kunizuia na
kukaa mbele ya gari yangu.
3) Tulipokwenda eneo la kukutania na
mara hii ilikuwa ni nje jirani ya jengo la utawala wanafunzi
walikusanyika wakimsubiri Mkuu wa Mkoa na kabla hajafika nilitwa na yeye
mwenyewe ili tuweke msimamo wa pamoja kama viongozi lakini badala yake
alitumia Polisi kunitisha na kuhaidi kuwa nitamtambua kuwa yeye ni
Serikali ,tulitofautiana tena nilipokataa hofu hiyo na ghafla tuliamua
kwenda eneo la kuongea na wanafunzi na ndipo yafuatyo yalitokea “
Mkuu wa Mkoa wakati anaanza kuongea alianza kusema maneno yafuatayo “
Mnaona hiki Kifua na huu mwili wangu , na hapo ndipo hali ilipochafuka
na kuamsha vurugu kubwa kutoka kwa Wanafunzi waliokerwa na kauli yake na
Polisi wa walimchukua na tafrani kati ya Polisi na Wanafunzi ikapamba
moto hali iliyosababisha mabomu ya machozi kulipuliwa kwa wingi kila
kona ya chuo na kila mtu kuanza kukimbia kuangalia usalama wake nikiwemo
mimi .
Nimesikiliza Mkutano wake na Waandishi wa Habari na leo
nimesoma nakusikiliza vyombo mbali mbali vya habari kwamba ninatafutwa
na Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa , nimeshangaa sana japo sio
kumshangaa Mkuu huyu wa Mkoa kwani ufahamu na uwezo wake naujua ulivyo
katika kufikiri na kutatua mambo ya msingi na muhimu , kwa jinsi
nilivyomsikia na kumuona alivyokuwa anashughulikia tatizo lile
lililotukutanisha jana pale Chuoni , kwa kweli nilishangazwa sana na
kuogopa kama hekima ya Mkiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
angeweza kushughulikia tatizo lile kwa namna ile ya Kiburi , Dharau na
Majivuno ambayo hakika ilikuwa ni chanzo cha wanafunzi kukataa
kumsikiliza na ndipo alipoamua kuondoka huku zomea zomea ikiendelea
kushamiri vizuri . Mabomu yalianza kupigwa , wanafunzi walipigwa na
kunyang’anywa pesa , simu , na lap top na vitu mbali mbali ambavyo
Polisi walikuwa wanaona vina thamani kwao , nilikuwa ninatazama mambo
haya huku roho yangu ikiwa inauma sana kwamba wanaopaswa kulinda usalama
wa raia na mali zao ghafla waligeuka kuwa vibaka wa kuumiza raia na
kupora mali zao .
Ninawapa pole wanafunzi kwa msiba wa rafiki
yao na siku ya jana ilikuwa ni siku ya Serikali kutumia busara kurudisha
matumaini kwa wanafunzi wale pamoja na raia , lakini badala yake wafiwa
walipotaka kudai haki zao za kulindwa , walipigwa , walidhalilishwa na
Chuo chao kufungwa bila sababu ya msingi wala kuzingatia mambo muhimu .
Ifahamike kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha kina wanafunzi kutoka sehemu
mbalimbali za nchi hii, na amri ya mkuu wa mkoa kufunga chuo na kuamuru
wanafunzi watawanyike ifikapo saa kumi na mbili jioni , huu ni ukosefu
wa upendo , hekima , busara na utu ikizingatiwa kuwa sababu na mchochezi
wa vurugu hizi ni Mkuu wa Mkoa kukosa maarifa na hekima.
Nimepokea ujumbe katika simu yangu kutoka kwenye simu yangu ya kiganjani
kutoka kwa Mkuu wa Mkoa inayonitishia na kuweka maisha yangu kwenye
hali ya hatari na ujumbe huo unasema “ UMERUKA KIHUNZI CHA KWANZA ,
NITAKUONYESHA KUWA MIMI NI SERIKALI ULIKOJIFICHA NITAKUPATA NA NITAKUPA
KESI NINAYOTAKA MIMI “ Mwisho wa kunukuu .
Mwisho, Ninamshukuru
kijana aliyerekodi tukio lote kuanzia mwanzo mpaka mwisho na hivi
tutanza kusambaza video cd hizo Nchi ili watanzania wajue ukweli na Mh
Rais aone utendaji mbovu wa wateule wake na vile nilitake Jeshi la
Polisi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria , maadili ,taratibu na kanuni
za kazi na sio kuendesha Jeshi kwa matakwa ya kisiasa , kufanya hivi ni
kuhatarisha usalama na utulivu wa Nchi yetu .
“ Che Guavera alisema “ if you tremble indignation at every injustice then you are a comrade of mine “
Wanafunzi jipeni moyo bado kitambo kidogo Taifa hili litabadilika .
No comments:
Post a Comment