http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Saturday, April 27, 2013

Kocha Yanga apewa nafasi ya Micho Rwanda


KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts ni kati ya makocha wanaopewa nafasi ya kuwania nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) zimeeleza, Brandts ni kati ya wanaopewa nafasi ikiwa ni siku chache baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu Sredojevich Milutin ‘Micho’ kufukuzwa kazi.
Micho raia wa Serbia aliyewahi kuwa kocha wa Yanga alitupiwa virago baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwa miezi minne mfululizo.
Brandts raia wa Uholanzi, amekuwa akipewa nafasi hiyo baada ya kamati ya ufundi ya Ferwafa kutoa pendekezo kutokana na mafanikio aliyoyapata wakati akiwa nchini Rwanda akiinoa APR.
“Unajua kocha (Brandts) kazi yake ilionekana wakati akiwa hapa, alichukua makombe sita kwa misimu miwili, pia anaujua mpira wa Rwanda na alishirikiana vizuri na watu wengi.
“Lakini ni kocha ambaye amecheza soka na kazi yake ilikuwa kwa mpangilio mzuri sana, tunaamini hata APR asingeondoka lakini uamuzi wa APR kutumia makocha wazawa ndiyo ulimuondoa,” kilieleza chanzo.
Alipoulizwa Brandts, jana kwamba kama aliomba kazi Rwanda au alikuwa tayari kujiunga na Amavubi alisema: “Ni suala la mchakato, waache kwanza wafanye kazi yao. Mimi ni kocha na ninapenda kufanya kazi yangu kwa mafanikio zaidi.”

No comments:

Post a Comment