http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Saturday, April 27, 2013

ALIYEFUFUKA GEITA AZUA KIZAAZAA


Mwanamke anayedaiwa kufariki miaka mitano iliyopita na kuonekana akiwa hai katika eneo la Kasamwa mjini Geita, amezua kizaazaa kikubwa mjini hapa.
Imedaiwa kuwa Flora Onesmo, (45) alifariki Februari 28, 2008 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa kijijini Nakasenya, Kata ya Butundwe lakini katika hali ya kushangaza, alfajiri ya Ijumaa iliyopita alikutwa ameketi nje ya nyumba ya dada yake aitwaye Monica James.
Mtu wa kwanza kumuona Flora ni Monica Onesmo ambaye alipotoka nje saa 11:00 alfajiri, alimwona mwanamke ameketi nje ya nyumba hiyo, akiwa anafanana sana na marehemu Flora.
Baada ya kumuona, aliwaita ndugu zake wengine akiwemo baba mzazi wa marehemu, James Tunge. Baba huyo alienda kuchukua picha ya marehemu mwanaye na kuanza kumfananisha ambapo ilibainika kuwa anafanana naye kwa kiasi kikubwa isipokuwa wanatofautiana makovu ya usoni ambapo marehemu alikuwa nayo mawili lakini mwanamke huyo analo moja.
Alipohojiwa, mwanamke huyo alisema kwamba alitokea porini Katoro, nyumbani kwa mganga wa jadi ambaye hata hivyo hakumtaja kwa maelezo kwamba majini yamemkataza.
“Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji, akaja mwanaume mmoja wakati nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa kwenye gari na watu wawili ambao sikuwatambua, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume mpaka hapa Kasamwa, tukashushwa saa 1:00 jioni,” alisema Flora.
Flora aliongeza kuwa ana ndugu zake Sengerema na Geita na kwamba kabla ya kutoweka, alishazaa watoto watano (idadi ambayo ni sawa na ile aliyoacha marehemu Flora), lakini alipoambiwa awataje alikuwa akichanganya majina.
Ndugu wa mwanamke huyo wanahusisha tukio hilo na ushirikina kwa kusema kwamba huenda ndugu yao alichukuliwa kwa njia za giza, lakini Mungu amemwezesha kurejea katika maisha ya kawaida.
Mmoja wa ndugu hao aitwaye Jubili alisema kifo cha Flora miaka mitano iliyopita kilikuwa cha kutatanisha, kwani aliugua ghafla baada ya kula viazi vitamu kwenye mji wa jirani na akaanza kuvimba tumbo kisha akafariki dunia.
Suala hilo lilifikishwa polisi ambapo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Japhet Lusungu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba ndugu zake waliondoka naye.

No comments:

Post a Comment