RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa bado ni dhamira
ya Serikali yake kuileta moja ya timu za Ligi Kuu ya Soka ya Hispania
(La Liga) kutembelea Tanzania na amemtaka Balozi mpya wa Hispania
katika Tanzania kusaidia kufanikisha dhamira hiyo.
Aidha, Rais Kikwete ameipongeza Hispania kwa kutetea ubingwa wa Kombe
la Mataifa ya Ulaya (Euro) 2012 katika mashindano yaliyomalizika mwezi
uliopita nchini Poland na Ukraine.
Akizungumza na Balozi mpya wa Hispania, Mheshimiwa Luis Manuel Cuesta
Civis mara baada ya kupokea hati yake ya utambulisho katika hafla fupi
iliyofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais alisema:
“Wananchi wa Tanzania, ambako timu za Hispania, zina washabiki na
wafuasi wengi, bado wanasubiri kwa hamu ziara ya moja ya timu kubwa za
Ligi Kuu ya Soka ya Hispania. Tunataka ije hapa, icheze mechi moja ama
mbili na itembelee mbunga zetu maarufu za wanyama,” alisema Rais
Kikwete na kuongeza:
“Kama utakavyokuja kuthibitisha mwenyewe, Watanzania ni watu wanaopenda
michezo na hasa soka na ni wafuatiliaji wakubwa wa Ligi Kuu ya
Hispania ambako timu zenye mvuto zaidi ni Real Madrid na Barcelona.”
Rais Kikwete pia aliipongeza Hispania kwa kutetea ubingwa wake wa Ulaya.
“Tunawapongeza sana kwa kuweka historia. Kwanza mlishinda Kombe la
Mataifa ya Ulaya, kisha mkashinda Kombe la Dunia. Sasa mmeweza kutetea
Kombe la Ulaya. Hili halijapata kutokea kwa nchi moja kushikilia
vikombe vyote viwili vikubwa vya soka duniani kwa wakati mmoja ama nchi
kutetea Kombe la Ulaya.”
No comments:
Post a Comment