Binti anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi
na mwajiri wake, Yusta Lucas (kushoto) akilia pamoja na mama yake, Modesta
Simon katika Hospitali ya Mwananyamala jana, baada ya mama yake kuwasili kutoka
Tabora ili kumjulia hali.
Kelele za vilio jana zilisimamisha kwa muda shughuli katika
Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam baada ya mama
mzazi wa msichana, Yusta Lucas (20) anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na
kuchomwa kwa pasi mwili mzima kumwona mwanawe kwa mara ya kwanza.
Zilikuwa dakika 10 ngumu kwa mama huyo, Modesta Simon
kuamini hali aliyomkuta mwanaye aliyelazwa hospitali hapo kuuguza majeraha
kutokana na kufanyiwa ukatili na
tajiri yake Amina Maige.
Mwanamke huyo anashikiliwa katika Kituo cha polisi Oysterbay
kwa tuhumu hizo na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Thobias Edoyeka
alisema leo atafikishwa mahakamani... “Bado sijafahamu kama atapelekwa ama
Kisutu au Kinondoni.”
Mara baada ya mama huyo kuingia katika wodi hiyo, Yusta
aliyekuwa ameketi kitandani aliruka na kumkimbilia mlangoni na kilichofuata ni
vilio.
Akizungumza huku akitokwa na machozi, Modesta alisema:
“Jamani Amina kweli amekufanya hivi, kila nikiuliza wananiambia hujambo kumbe
umeharibika hivi...”
Alisema habari za mateso na kulazwa kwa mwanaye alizipata
kutoka kwa ndugu yake anayeishi Arusha.
“Alhamisi nilipata simu kutoa kwa ndugu yangu Marieta
Shitindi yeye anakaa Arusha, akaniambia ameona kwenye Mwananchi na runinga
kwamba Yusta amelazwa baada ya kupigwa na Amina ndipo nikafunga safari kutoka
Tabora kuja kuhakikisha.
Amina ni mtoto wa mjomba wangu kabisa na sikuwahi kuambiwa
chochote, niliamini wanaishi vizuri na sikudhani kama anaweza kulifanya jambo
hili.”
Modesta alisema awali alikuwa na mawasiliano na mwanaye
kupitia simu ya mama yake Amina ambaye wanaishi karibu, lakini hivi karibuni
alianza kupata wasiwasi baada ya kila alipohitaji kuongea naye alipatiwa sababu
hivyo akaomba Yusta kurudishwa na aliahidiwa angepelekwa mwezi huu.
“Aliniahidi mwezi huu atamleta Yusta nyumbani alisema
anataka muda amnunulie na cherehani ili akija apate shughuli ya kufanya...”
alisema.
Ofisa Muuguzi katika wodi aliyolazwa Yusta, Erica Massawe
alisema hali ya binti huyo imeimarika na alisharuhusiwa kutoka tangu Ijumaa
iliyopita na kwamba wanasubiri maelekezo ya Polisi na Ustawi wa Jamii kwani
ndiyo wahusika wakuu.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment