http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Wednesday, September 4, 2013

WACHUNGAJI WAONESHANA JEURI YA FEDHA KWENYE MSIBA WA MOSES KULOLA

Stori: Haruni Sanchawa na Gladness Mallya
MAZISHI ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God Tanzania, Dk. Moses Kulola yamezua mambo baada ya baadhi wachungaji wa makanisa mengine waliofika kuuaga mwili wake kufanya mambo yaliyotafsiriwa na baadhi ya waombolezaji kuwa ni kuoneshana jeuri ya fedha, Uwazi lilikuwepo.
Jeneza la mwili wa marehemu likiwa mbele ya waombolezaji.
Shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu huyo aliyefariki dunia Agosti 29, 2013 ilifanyika Agosti 31, 2013 kwenye viwanja vya Kanisa la EAGT, Temeke, jijini Dar es Salaam ambapo pia watumishi hao wa Bwana wengi wao waliwasili na magari ya kifahari huku kila mmoja akionekana kumfunika mwenzake kwa uzuri wa magari hayo.
Mchungaji, Anthony Lusekelo akisaini kitabu cha maombolezo.
Ilikuwa wakati wachungaji na maaskofu wa makanisa mbalimbali nchini walipopewa nafasi ya kumzungumzia marehemu, wengine walitamka rambirambi zao papo hapo na ndipo jeuri ya fedha ilipoonekana.
Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni Assemblies of God, Dar, Dk. Getrude Pangalile Rwakatare alitangaza rambirambi yake kwa kusema anatoa shilingi milioni moja.

Mama Getruda Lwakatare  akisaini kitabu cha maombolezo.
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar, Josephat Gwajima ‘alimpiga kumbo’ Mama Rwakatare  baada ya kushika kipaza sauti na kutamka bayana kwamba kutokana na kifo hicho, yeye ameamua kutoa shilingi milioni kumi (10,000,000/=) kama rambirambi kwa familia ya Askofu Kulola.
Gwajima akasindikiza na maneno kwamba, anahisi furaha ya aina yake kusikia kuwa asilimia kubwa ya watumishi wa Mungu nchini wamepita mikononi mwa Dk. Kulola, akawataka  viongozi wote wa dini kufuata  nyayo zake  kwa manufaa ya nchi.
Baada ya Gwajima kutangaza ‘mzigo mnene’ wa rambirambi,  alifuatia Mchungaji Anton Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ ambaye kabla ya kutamka atatoa kiasi gani alisema Gwajima amekwenda mbele sana, amemuweza, lakini yeye atakwenda mbele zaidi yake.

Mchungaji Josephat Gwajima akitoa salamu za rambirambi.
Baadhi ya waombolezaji walianza kutoa maneno ya chini kwa chini ‘wakitabiri’ kuwa, Mzee wa Upako angefurukuta sana angetoa shilingi milioni kumi na moja, lakini hali haikuwa hivyo.
Msikie Mzee wa Upako: “Gwajima ameniweza kweli kwa kuwa yeye ametoa milioni kumi, sasa mimi natoa milioni kumi na tano (15,000,000/=).”
Baada ya watumishi hao kutangaza rambirambi hizo baadhi ya waombolezaji waliohudhuria ibada hiyo walianza kunong’ona wakisema kuwa wachungaji hao waliamua kushindana kwa kuoneshana nani zaidi kwani wengi walifika na magari ya bei mbaya na sasa wanatangaza ‘mzigo mrefu’ kwa ajili ya rambirambi.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa wachungaji na maaskofu wengine waliamua kufanya siri rambirambi zao kwa vile ndivyo walivyojisikia.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel & Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe.
Watumishi ambao walipata nafasi ya kusema lakini hawakutangaza rambirambi zao hadharani ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel & Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, Askofu Sylvester Gamanywa ambaye pia ni Rais wa Wapo Mission International, Askofu David Mwasota wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly, Nabii wa Kanisa la Living Water ‘Makuti Kawe’, Onesmo Ndegi, Mchungaji Florian Katunzi wa Kanisa la EAGT City Center na wengine wengi.
Kwa upande wake, Askofu Kakobe aliwataka waumini wa Kanisa la EAGT kusimama imara ili kuweza kudumisha amani na mshikamano ndani ya kanisa hilo na taifa kwa jumla kama alivyokuwa mwasisi wao, marehemu Kulola.
“Kutangulia kwa kamanda wetu Kulola kusiwe mwisho wa ushirikiano kati yenu wenyewe kwa wenyewe na makanisa mengine bali muendelee kudumisha yale aliyoyaacha,” alisema Kakobe alipopewa nafasi ya kusema ni jinsi gani alivyomfahamu Kulola.

Maaskofu na wachungaji wakiupokea mwili wa marehemu.
Mama Rwakatare aliwashtua wengi pale alipoanika matatizo yake ya ndoa na aliyekuwa mumewe, marehemu Rwakatare.
Alisema wakati wa matatizo ya ndoa yake, Askofu Kulola alimuombea mara nyingi huku akimfundisha Neno la Mungu na kumwambia kuwa hanyanyaswi yeye bali ni Yesu Kristo.
“Baada ya kuniombea, Kulola alikuwa akiniandikia barua kila mwezi ya jinsi ya kumwomba Mungu mpaka matatizo ya ndoa yangu yalipokwisha na hadi leo hii ninaishi bila kuwa na hofu, pia nimekuwa mchungaji kwa sababu ya mafundisho ya Jemedari Kulola, kama si yeye nisingekuwa hapa nilipo,” alisema  kwa majonzi makubwa Mama Rwakatare ambaye kanisa lake ni maarufu kwa jina la Mlima wa Moto.
Mazishi ya marehemu Kulola yanatarajiwa kufanyika jijini Mwanza kesho Jumatano.   Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.

                           source::::GPL

No comments:

Post a Comment