http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Friday, September 13, 2013

MFUNGWA AHITIMU DARASA LA SABA DAR..

 
Serikali imempa fursa ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu, mfungwa wa Gereza la Watoto lililopo jijini Dar es Salaam baada ya kumruhusu kufanya mitihani ya taifa ya darasa la saba kwenye Shule ya Msingi Ukonga.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Yusufu Kipengele, jana alisema kuwa amefanikiwa kuhitimu darasa la saba jana baada ya kuungana na wanafunzi wengine nchini kufanya mitihani hiyo akiwa chini ya ulinzi  wa askari magereza na wa polisi kuanzia juzi.

Alisema wakati anahukumiwa kwenda jela, alikuwa ni mwanafunzi wa shule moja ya msingi iliyopo wilayani Kibaha.

Alisema alisajiliwa kufanya mitihani yake katika shule hiyo na kwamba kutokana na umbali, aliombewa kuifanyika katika Shule ya Msingi Ukonga ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Alisema wakati akihukumiwa kwenda jela, namba yake ya kufanya mtihani ilipelekwa Mei mwaka huu kwenye shule aliyokuwa akisoma.

“Mwezi Mei huwezi kufanya mabadiliko ya vituo ila kutoa taarifa baraza la mitihani kama kuna tatizo kama hilo na kama kuna haja ya kulitatua kwa vyote inavyoona inafaa,” alisema.

Alisema baada ya baraza kupelekewa taarifa kuhusiana na mtahiniwa huyo liliagiza mkoa wa Pwani umtafutie shule iliyopo jirani na gereza hilo ili afanye mitihani hiyo.

Kipengele alisema kuwa baada ya kupata shule hiyo, mitihani yake ilifungwa kwenye bahasha ya peke yake na kupelekwa Kibaha kisha kupelekwa Shule ya Msingi Ukonga ambako aliruhusiwa kuifanya.

Alisema baada ya kufanya mitihani hiyo, ilipelekwa Kibaha kwenye shule alikokuwa akisoma na kuunganishwa na ya wenzake na kupelekwa kusahihishwa.

Alisema kwa siku mbili mfululizo mfungwa huyo alikuwa akitokea kwenye gereza hilo kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 12, mwaka huu na kupelekwa na askari hao kwenye kituo chake cha kufanyia mtihani na kurudishwa gerezani.

Alisema alihukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wilayani Kibaha mapema mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu hatima yake ya kuendelea na masomo ya sekondari endapo atafaulu mitihani hiyo, alisema atalazimika kusubiri amalize kifungo.

Vilevile alisema kuwa wanafunzi 19 wenye ulemavu wa uoni hafifu nao ni miongoni mwa waliofanya  mitihani hiyo mkoani Pwani.

Kipengele alisema kuwa hakuna taarifa zozote za kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu vilivyoripotiwa kutokea.

No comments:

Post a Comment