Kikosi cha FFU uwanjani. Jeshi la polisi mkoani Morogoro limekanusha madai ya kuhusika na kumpiga risasi begani, katibu wa jumuiya na taasisi ya kiislamu nchini, sheikh Ponda Issa Ponda, na kwamba iwapo sheikh huyo anaamini kufanyiwa hivyo, ajitokeze na kuthibitisha kauli hizo ambazo zimeendelea kutolewa na wafuasi wake.
Akizungumzia tukio la vurugu zilizojitokeza baada ya kufanyika kwa
mhadhara wa baraza la Iddi, lililoandaliwa na wahadhiri wa kiislamu wa
mkoa wa Morogoro eneo la Kiwanja cha ndege,na baadaye kuzagaa kwa
taarifa kuwa sheikh Ponda amepigwa risasi na kujeruhiwa, kamanda wa
polisi mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile, amesema saa chache kabla ya
mhadhara kumalizika, sheikh Ponda alijitokeza na kuzungumza na
wananchi, na baadaye kuondoka na gari, akisindikizwa na kundi la wafuasi
wake waliokuwa kwa miguu, lakini polisi walimzuia kwa mbele katika
barabara ya Tumbaku, kwa nia ya kutaka kumkamata kutokana na tuhuma za
uchochezi katika mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar, jambo
lililosababisha wafuasi hao kuwazuia polisi kwa mawe na kusababisha
watumie risasi baridi kupiga hewani kuwatawanya.
Kuhusu kushindwa kumkamata sheikh Ponda wakati akiwa jukwaani,
Shilogile amesema ilikuwa ni kuepusha vurugu ambazo zingeweza
kujitokeza,ambapo mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 3,000 .
Wakizungumza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa morogoro,baadhi
ya wazazi waliolazwa na watoto katika wadi namba 06, wamesema Jumamosi
jioni vurugu kadhaa zilijitokeza baada ya kuwasili kwa majeruhi sheikh
Ponda hospitalini hapo,ambapo kabla ya kupata huduma, aliondolewa na
watu waliokuwa na pikipiki.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kwa wafuasi wake na
waandaaji wa mhadhara huo, zimebainisha kuwa sheikh Ponda anaendelea
vyema jijini Dar es Salaam alikopelekwa,baada ya zahanati mbili tofauti
alizopelekwa awali kuonekana kukosa huduma zilizomstahili,na alipewa
huduma ya kwanza ya kuongezewa maji na damu akiwa kwenye gari, na
baadae kuondolewa risasi mbili anazodaiwa kupigwa kwenye bega.
No comments:
Post a Comment