Mnyika aitwa Ikulu, JK awakumbuka Mabwepande
HOJA ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) kuhusiana na suala la
tatizo la upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, inaelekea
kupata ufumbuzi kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumuita Ikulu mbunge
huyo Jumatatu wiki ijayo.
Wengine walioitwa kukutana na rais ni Mkuu wa Mkoa, Mecky Sadick, wakuu
wote wa wilaya pamoja na wabunge na wataalamu kutoka Wizara ya Maji.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa daraja la Mtaa
wa Golani, Kata ya Saranga, Rais Kikwete alisema kuwa kutokana na
wananchi wa kata hiyo kupiga kelele kuhusiana na suala la maji ameamua
kukutana na viongozi hao ili kupatiwa ufumbuzi.
Kikwete pia alitaka kuwepo na mfumo maalumu wa mabomba ya maji
yatakayojengwa kwa saruji kutoka Ruvu Chini na kuja jijini Dar es Salaam
moja kwa moja bila kuchepuliwa sehemu yeyote.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alikiri kuwepo kwa wizi wa maji katika maeneo ambayo mabomba ya maji yamepita.
“Watu wasifanye ukanjanja katika masuala ya maji, mabomba yanatandazwa
na watu wanaiba maji, shida inayotokea ni maji hayo kutokufika jijini
Dar es Salaam,” alisema.
Alifafanua kuwa lita milioni 65 zinahitajika ili kukabiliana na tatizo
la maji na kwamba upanuzi wa Ruvu Juu na Chini ujenzi wake utakamilika
Julai na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kuhakikisha maji
yanapatikana kwa haraka ili kumaliza tatizo.
Hatua ya Mnyika kuitwa Ikulu imetokana na kusimama kidete katika suala
la maji ambapo Aprili 4, mwaka huu aliwasilisha hoja binafsi na kuitaka
serikali kuchukua hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi
na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam hoja ambayo
ili iliondolewa bungeni kibabe.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemaliza kilio cha muda mrefu kwa wakazi
604 wa mji mpya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni kwa kumpa kila mmoja
mifuko 100 ya saruji itakayogharimu sh milioni 840.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Home Shopping Center (HSC), Ghalib
Mohamed, aliahidi kutoa mabati 30 kwa kila mkazi ili waondokane na
kuishi kwenye mahema yaliyotoboka.
Rais alikuwa katika mwendelezo wa ziara yeka mkoani hapa kukagua
shughuli za maendeleo ambapo pia alifungua shule ya msingi, kituo cha
polisi, nyumba za walimu na polisi vilivyojengwa kwa ushirikiano wa
Kampuni za HSC na TSN katika mji.
Wakazi hao ni wale ambao nyumba na mali zao zilizolewa na mafuriko mwaka 2011.
Rais alisema serikali imeamua kufanya hivyo baada ya kutembelea mahema
ambayo wanaishi kwa sasa na kubaini kuwa yametoboka na kwamba wakati wa
mvua wamekuwa wakiishi kwa taabu.
Alisema fedha hizo leo zitakuwa zimefika kwa mkuu wa mkoa ili waweze
kununuliwa saruji hiyo ambapo pia wakazi 21 kati yao walikabidhiwa hati
za makazi na rais huku akiagiza hati nyingine ziweze kukamilika haraka
iwezekanavyo.
Naye Mkurugenzi wa HSC, alisema kupitia sera ya kampuni yao watatumia
sehemu ya faida kuwasaidia wananchi mbalimbali waliokumbwa na matatizo
kwani ni vema kugawana na wasio nacho.
Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=46963
No comments:
Post a Comment