Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti
ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi
bungeni mjini Dodoma, imewang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara
zao zilishindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni
jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya
Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano
akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Dk Mathayo David Mathayo.
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni
Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa 2:09
usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo
iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni
Mbunge wa Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi ni
mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais
Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii,
yaliyotokea yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii
kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida
kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika
aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo
hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa ripoti
hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na
kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo
akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia
mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo ya wafugaji aliyopewa na Rais
Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa
mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi
(Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali
ushauri wa Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi
wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati yake,
Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na
Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea
kwenye mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya
wizara hiyo ni kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali
izichunguze simu zao kuanzia leo.”
No comments:
Post a Comment