Hatimaye
Mbunge Rosweeter Kasikila (60 - pichani), aliyefunga ndoa na kijana
mwenye umri wa miaka 26, amefunguka kwa kusema aliyeng'ang'ania kufunga
ndoa hiyo ni kijana mwenyewe licha ya kumtahadharisha tofauti ya umri
wao. Kasikila
alitoa kauli hiyo jana, baada ya kutakiwa kujibu shutuma zilizotolewa
na mumewe huyo, Michael Christian (26 - pichani) ya kung'ang’ania vyeti
vyake vya elimu kwa lengo la kumtaka arudi nyumbani.
Christian
aliyefika katika ofisi za NIPASHE jana alitoa nakala ya barua aliyoituma
kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuomba
atumie uwezo wake wa kisheria ili mbunge huyo amrudishie vyeti vyake
alinavyovishikilia.
Kufuatia
maelezo hayo, NIPASHE ilimtafuta Dk. Nchimbi kwa njia ya simu ili
athibitishe kupokea nakala ya barua hiyo lakini simu yake ilikuwa
imezimwa.
Nakala
nyingine za barua hiyo zilitumwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na
Haki za Binadamu kwa jamii-Madhehebu ya dini nchini, Askofu William
Mwamalanga, Mchungaji wa Kanisa la Assembilies of God, Mikocheni B,
Mchungaji Getrude Rwakatare na vyombo vya habari.
Akijibu
shutuma hizo, mbunge huyo alisema hajawahi kung'ang'ania vyeti vya
kijana huyo wala kulazimisha ndoa kama anavyodai Christian.
"Nahisi kuna
watu wanamtumia ili wanichafue, siwezi kung'ang'ania vyeti, kwanza vya
kazi gani kwangu, ukweli ni kwamba Michael, shida yake anataka
nichafuliwe, kwangu aliondoka wakati sipo, sasa hivyo vyeti
nimeving'ang'ania saa ngapi," alisema na kuongeza:
"Mwaka jana
nikiwa Dodoma nilipata taarifa ameondoka nyumbani, kweli nilivyorudi
nilikuta amechukua vitu vyake vyote kasoro tu vile nilivyomnunulia,
hivyo vyeti anavyosema nimeving'ang'ania mbona hajawahi kutamka mbele
yangu zaidi nimeona kwenye magazeti," alihoji.
Alisema
baada ya kufika nyumbani alipata taarifa kuwa, mume wake huyo amepanga
chumba na anaishi na mwanamke mwingine (askari) ambaye ni mjamzito.
Alisema
utaratibu alioutumia kijana huyo wa kumchafua kwenye magazeti siyo
sahihi na kumshauri angeenda mahakamani au kanisani kama aliona haitaki
ndoa tena.
Aliongeza kuwa yeye na Christian walifahamiana mwaka 2009 baada ya kufiwa na mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mushi.
"Sikumtongoza
kama anavyosema, alikuja katika hospitali ya Bagamoyo akitokea chuo cha
Red Cross wakati huo nilikuwa Muuguzi Mkuu, aliponiona alinipenda
alianza kunitongoza, nilimkatalia na kumwambia mimi ni mtu mzima sana
kwake, " alisema na kuongeza: "Alikuwa
ananitumia email (barua pepe) za kunitaka, nilimwambia umri wangu ni
mkubwa, lakini yeye alikuwa ananiambia kwenye vitabu vya dini kuna
sehemu gani kumeandikwa umri," alisema.
Alisema alijikuta ametumbukia kwenye penzi la kijana huyo na kuanza mahusiano naye.
"Nina nakala
zote za vidhibitisho ambavyo alikuwa akinitumia kunitongoza
nimevichapisha kama vielelezo vyangu, tena wakati tumeanza uhusiano
Taasisi ya Safina ambayo ilikuwa ikimsaidia katika masomo yake,
ilinipigia simu," alisema na kuongeza: "Safina
walitaka kujua kama nina mahusiano na huyu kijana niliwajibu ni kweli,
waliniambia kama ndiyo hivyo wanafuta kumsaidia kwa sababu wao
huwasaidia wale ambao hawana uwezo, yatima, " alisema.
Alisema wakati taasisi hiyo ikimfuta, ilikuwa imemlipia Christian sehemu ya ada ya masomo aliyokuwa akiyachukua."
"Nililazimika
kumlipia ada ya mwaka wa pili na watatu wa masomo yake pamoja na mambo
mengine na ilifika kipindi aliniambia anataka kunioa, ndipo tulipofanya
mchakato ambapo nilitolewa mahari na ndoa ilifuata taratibu zote ikiwa
ni pamoja na kutangazwa mara tatu," alisema.
Alisema
Christian alifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutoa mahari ya Sh.
200,000 na baada ya harusi alipelekwa Kondoa kwa ndugu wa kijana huyo.
"Huko
tulienda kati ya mwezi Julai au Agosti, mwaka jana, tulifanyiwa sherehe
za kimila na ndugu za mume wangu ambao ni baba mdogo, bibi mzaa baba
yake na shangazi, pia ndugu zake wa Kimara na Dodoma wananijua, "
alisema.
Hata hivyo,
mbunge huyo alipoulizwa kama ndoa hiyo ipo sasa hasa kufuatia shutuma
hizo, alisema hawezi kujua kwa sababu mume wake aliondoka bila kumuaga
na kwa sasa anaishi na mwanamke mwingine toka Novemba mwaka jana.
Alisema
wakati wa mahusiano yao wafanyakazi wenzake Christian walikuwa wakimhoji
kwa nini ameamua kuwa na mtu mzima kama (mbunge), lakini yeye aliwajibu
hakuna umri kwenye biblia.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kuchukua hatua dhidi ya kijana huyo, mbunge huyo alisema hana mpango.
Mbunge huyo
alijitetea kuwa, hakumlazimisha kufunga ndoa na kwamba wakati kijana
huyo akimtongoza, alimweleza kuwa hawezi kuzaa kwa sababu umri wake
umeshapita.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment