Ndugu
zangu, lazima ieleweke kuwa kugombana ni sehemu ya maisha ya binadamu.
Yawezekana kabisa ulikuwa na mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako
wote na sasa mmeachana baada ya kutofautiana.
Kutengana kuna mambo
mengi, wakati mwingine inaweza kuwa chanzo cha yote hayo ni hasira tu.
Siku zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi
yake halisi ya kufanya maamuzi.
Hapo ndipo kwenye lengo la mada yetu
ya leo. Kwamba kwa msingi huo umegundua kwamba kumbe mpenzi wako
uliyeachana naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa
akiyafanya, ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala
yake mnaweza kukaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza. Yes! Hilo
ndilo ninalotaka kulizungumzia. Tuendelee kujifunza.
NI SAHIHI?
Baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine
kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha.
Kwamba hakuna mwanaume wala mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa
naye tofauti na huyo anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo,
kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni
kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo
mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana
taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana
na mpenzi wako wa zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha,
hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda
jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye
ndoa.
FAIDA ZAKE NI HIZI
Utafiti usio rasmi nilioufanya, unaonesha
kwamba zipo faida za kurudiana na mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni
awe moyoni mwako.
Hebu msikie Julius Kihesupe wa Uwanja wa Ndege,
jijini Dar es Salaam, ambaye alipata kuzungumza nami hivi karibuni
akitoa maoni yake kuhusu suala hili: “Si vibaya kurudiana, maana kwanza
mnakomaza uhusiano.
“Kumrudia mtu wako wa zamani maana yake ni kwamba
umekubaliana na udhaifu wake wote. Unajua anachopenda na anachochukia,
hapo lazima mtadumu. Bila kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu,
tukiwa na miaka miwili kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila
mmoja alikaa kivyake kwa miezi kama sita hivi, nikakutana naye Dar,
nikiwa nimeachana naye Mbeya, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi
minne mbele yake tukafunga ndoa.”
Umeona mambo hayo? Sasa basi, ikiwa
unahitaji kurudiana na mwenzi wako wa zamani, dondoo zifuatazo hapa
chini zitakuwa msaada wako mkubwa sana.
CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuchunguza
ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema hivyo kwa sababu
yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua anapopatikana ni mwanzo wa
kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika himaya yako.
ANA HISTORIA GANI?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano
baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya ‘ushushushu’ wako
kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’ sana, maana yake
ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili
na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda
huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano
mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uhairishe
zoezi lako.
Natamani kuendelea kuzungumza nanyi rafiki zangu, lakini nafasi yangu kwa leo imeishia hapa.
Wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mwendelezo wake, USIKOSE!
No comments:
Post a Comment