http://s3-us-west-2.amazonaws.com/millard-ayo-bucket/wp-content/uploads/2017/09/12124853/Kubenea.jpg

Tuesday, July 23, 2013

JINSI YA KUGUNDUA NA KUANZISHA UHUSIANO ULIO SAHIHI

LEO nakwenda kuhitimisha mada yetu iliyodumu hapa kwa wiki nne sasa. Ni mada yenye maana sana katika maisha ya uhusiano. Wengi wamejikuta wakiingia kwenye matatizo kwa kutokugundua uhusiano ulio sahihi.

Haya ni matatizo makubwa sana lakini ni afadhali kwako ambaye umepata bahati ya kukutana nami katika ukurasa huu maana unakwenda kutengeneza kitu kikubwa katika maisha yako.
Tumeshaona mengi ya kufanya hasa kwa wale ambao wapo nje ya uhusiano, sasa basi leo tunaangalia zaidi upande wa ndani ya uhusiano. Hebu twende tukaone...

NDANI YA UHUSIANO
Hapa ndipo kwenye matatizo zaidi lakini ikiwa utakuwa makini katika kufuatilia kipengele hiki, utaondokana na tatizo hilo kwa urahisi zaidi.
Inawezekana mpenzi wako anakunyanyasa, masimango kila siku hayaishi, amekuwa mtu wa maneno madogomadogo, wakati mwingine ni kama anakuambia amekuchoka.
Huna haja ya kujiumiza; kwa nini uendelee kuutesa moyo wako kwa mtu ambaye haonyeshi kujali chozi lako? Hebu fuatilia dondoo zifuatazo kwa makini, utaweza kung’amua jinsi ya kufanya.

(i) Chunguza mwenye matatizo
Vituko vya mpenzi wako vinaweza kukuchosha na kufikia hatua ya kuchukia kuendelea na uhusiano naye.
Pamoja na hayo inawezekana moyo wako ukawa unampenda kwa dhati na ukawa haupo tayari kuachana naye. Hapa unatakiwa kwanza uchunguze ni nani mwenye matatizo kati yako wewe na yeye.
Kuchunguza kwanza kutakufanya wakati unatoa maamuzi, yawe sahihi zaidi kuliko kuamua kabla ya kujua nani mwenye matatizo.
 Najua hili linaweza kukushangaza kidogo, huna sababu ya kushangaa, inawezekana matatizo yaliyopo katika mapenzi yenu yanasababishwa na wewe.

(ii) Tafuta suluhu

Ikiwa uligundua kwamba mpenzi wako ndiyo chanzo cha matatizo, anza kutafuta suluhu! Panga kutoka naye, kisha zungumza naye ukitumia kauli ya upole na unyenyekevu.
Mweleze unavyochukizwa na tabia zake na jinsi anavyokusababishia simanzi ya moyo wako. Uwazi wako ndiyo silaha yako kubwa katika kuweka mambo sawa, lakini ikiwa ataahidi kubadilika na baadaye akawa hana mabadiliko yoyote, njia inayofuata itakuwa muafaka sana kwako.

(iii) Ondoa sononeko

Huna sababu ya kuendelea kulea matatizo, kama unaona anazidi kukuumiza kila wakati ni wajibu wako kufanya maamuzi yatakayokuweka huru.
 Kuendelea kuwa na simanzi katika moyo ni sawa na kuruhusu kuwa katika utumwa wa mapenzi, jambo ambalo mwisho wake huwa mbaya.
Jiondolee sononeko moyoni mwako kwa kufanya maamuzi sahihi, amini Mungu amekuumba kwa makusudi, anajua mwenzi wako ni yupi.
Ikiwa huyo anakutesa achana naye, subiri yule aliyeumbwa kwa ajili yako anakuja.
Haya mambo yanawezekana, ni suala la kuamua kwa moyo na kuchukua hatua. 

No comments:

Post a Comment