ASALAAM
aleiykhum msomaji wangu, jina langu ni Chausiku Omar, al-maaruf Bi.
Chau. Ndiyo yuleyule mfundaji wako. Nitakuwa hapa kila siku kwa uwezo wa
Mungu ili kukupa somo, vilevile kujibu maswali yako. Lengo langu ni
moja tu, kukuwezesha wewe mwanamke mwenzangu kutulia kwenye ndoa au
penzi lako.
Mwanamke ndiyo dira ya mwanaume. Ukiona mumeo
hatulii, mwanaume wako anakuwa na hulka ya kurukaruka, jiangalie
mwenyewe mara mbili. Katika kila uhusiano wenye migogoro, ukiuchunguza
kwa makini unabaini uwepo wa upungufu mkubwa wa mwanamke katika
‘kumhendo’ mwanaume wake.
Mada yangu leo inahusu namna ya kumtuliza
mwanamke kiguu na njia. Shoga yangu, nataka kuanzia leo utambue kuwa
mwanaume si malaika. Kwa maana hiyo, unatakiwa ujue jinsi ya kucheza
naye kama binadamu. Acha kiburi, usizubae, msome vizuri kisha mpatie.
Atatulia tu.
Shosti, kumbuka kuwa unatakiwa kumbembeleza mumeo kwa
njia yoyote mpaka atulie. Mwanaume hauzwi dukani, ‘supermarket’ wala
hana bei. Ingekuwa anauzwa na bei yake inajulikana, kila mtu angekuwa
naye. Angetumia jeuri ya fedha kumpata anayemtaka.
Hebu shoga yangu
kaa na mshangao sasa, wanawake wengi tu tena wana fedha nyingi, wanaumia
upweke, hawana waume wa kutulia nao. Kama wewe unaye wako, tena bahati
nzuri mmefunga ndoa, hakikisha unamtuliza ili ufurahie maisha yako ya
kimapenzi.
TUMIA NJIA HIZI KUMWEKA SAWA MWANAUME WAKO
Kwanza
kabisa, unapoona mwanaume wako amekuwa kiguu na njia, yaani hatulii,
tafuta sababu zinazomfanya awe hivyo. Je, sababu ni wewe mwenyewe? Una
wivu sana, una mdomo mchafu, kiburi, huelekei anavyokuelekeza? Labda una
roho mbaya kwa ndugu zake. Tazama mambo hayo.
Hatua ya pili;
Ukishajichunguza, muombe mwanaume wako kikao ili mzungumzie matatizo
yenu. Usikae kimya wala usimwogope. Katika kikao hicho, mwache aongee ya
moyoni, nawe sema yako, mwisho utajua nani mwenye matatizo. Baada ya
hapo, fanyeni masahihisho. Ulipokosea omba msamaha.
Hatua ya tatu;
ikiwa katika mazungumzo umegundua mwanaume wako ndiye tatizo, mweleweshe
taratibu mpaka aelewe makosa yake. Achana na maneno ya watu wasiojua
thamani ya mume ambao hudiriki kusema: “Atajijua akitaka atasema na mimi
asipotaka aache mimi nd’o mkewe.”
Kasoro nyigine ni kwamba wapo
wanawake hutaka kuishi kwa mashindano na wanaume zao. Nawaombeni mashoga
zangu msifanye hivyo, mwanamke akiwa kiguu na njia, aibu yake ni kubwa
zaidi ya mwanaume. Uchafu wako, utamfanya yeye aonekane msafi wakati
ukweli naye hajatulia.
Pengine mwanaume wako hatulii nyumbani lakini
si kwa sababu ana wanawake wengine. Inawezekana ni mtu wa kuwaendekeza
marafiki, kwa hiyo wanakaa baa au maeneo mengine, wanazungumza mpaka
usiku wa manane ndiyo anarudi nyumbani.
Sasa ikiwa nawe utaanza
kuzurura halafu mna watoto, mtawalea saa ngapi? Nani atamrekebisha
mwenzake? Nakuhakikishia shoga, wewe ukiamua, mwanaume wako atatulia
nyumbani. Maneno yako mazuri na tabia yako njema, ni silaha.
WANAWAKE TUNAPOTEA
Bibie,
sisi wanawake wa siku hizi ni tatizo. Angalieni ndoa za zamani zilikuwa
zinadumu kwa sababu wanawake walikuwa wakifuata taratibu. Mke
anamuomba mume wake wakae na kutafuta suluhu pasipo hata jirani kujua.
Siku hizi, rafiki au shoga ndiyo wa kwanza kwenda kumhadithia na
kumuomba ushauri.
Ikiwa mtaweka vikao, hamtapigana hata kama mmoja
wenu atakuwa na jazba. Vizuri pia kuweka vikao kipindi ambacho kila
mmoja hasira zake zimepungua.
Bila mazungumzo hamtapata ufumbuzi,
wanaume wengine siyo waongeaji ila akishakasirika utaona tu amebadilika.
Sasa basi, kwa nini usimshawishi akwambie? Hiyo ni kazi yako,
atakwambia tu. Ukienda kumsimulia rafiki ndiyo utapata jawabu?
MWANAMKE NDIYO SERIKALI YA MWANAUME
Mwisho
kabisa nakutaka mwanamke ujitambue na uelewe nafasi yako ndani ya
nyumba. Mwanamke ndiyo serikali ya mume, usijaribu kukaribisha shetani
ndani ya nyumba. Endapo utampa maneno mazuri mumeo, wazimu wake wote
utaondoka. Shoga mwanaume ni kama mtoto. Ukimdekeza atadeka,
ukimbembeleza anabembelezeka, ukimchapa, atakuchukia.
Hata kama una
kazi, jaribu kupanga muda wa kumpikia mumeo, kumfulia nguo na
kumwandalia mambo megine muhimu ili ajisikie raha na ajivune kuwa na
mwanamke mzuri. Ukimwachia kila kitu afanye dada wa kazi, matokeo yake
hali ya hewa kuchafuka ndani ya nyumba.
No comments:
Post a Comment